Mathayo 23:29-38
Mathayo 23:29-38 SRUV
Ole wenu, Waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki, na kusema, Kama sisi tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii. Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii. Kijazeni basi kipimo cha baba zenu. Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya Jehanamu? Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulubisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji; hivyo ije juu yenu damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi, tangu damu ya Habili, yule mwenye haki, hata damu ya Zakaria mwana wa Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu. Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki. Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku awakusanyavyo pamoja vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka! Angalieni, nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa.