Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 22:7-23

Luka 22:7-23 SRUV

Ikafika siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja Pasaka. Akawatuma Petro na Yohana, akisema, Nendeni, mkatuandalie Pasaka tupate kuila. Wakamwambia, Wataka tuandae wapi? Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini mtakutana na mwanamume akiwa amebeba mtungi wa maji; mfuateni mkaingie katika nyumba atakayoingia yeye. Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Kiko wapi chumba cha wageni, nipate kula Pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu? Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, kimekwisha tayarishwa; andaeni humo. Wakaenda, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa Pasaka. Na saa ilipofika aliketi chakulani, yeye na wale mitume pamoja naye. Akawaambia, Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu; kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hadi itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu. Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi; Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hadi ufalme wa Mungu utakapokuja. Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.] Lakini, tazama, mkono wake yeye anayenisaliti upo hapa pamoja nami mezani, Kwa kuwa Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyokusudiwa; lakini, ole wake mtu yule amsalitiye! Wakaanza kuulizana wao kwa wao, ni yupi miongoni mwao atakayelitenda jambo hilo.

Soma Luka 22