Luka 20:27-47
Luka 20:27-47 SRUV
Kisha baadhi ya Masadukayo wakamwendea, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; na wa pili [akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto;] hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. Mwisho akafa yule mke naye. Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionesha katika sura ya Kichaka, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa maana kwake wote wanaishi. Waandishi wengine wakajibu wakamwambia, Mwalimu, umesema vema; wala hawakuthubutu kumwuliza neno baada ya hayo. Akawaambia, Wasemaje watu kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi? Maana, Daudi mwenyewe asema katika kitabu cha Zaburi, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kulia, Hadi niwaweke adui zako Kuwa kiti cha kuwekea miguu yako. Basi Daudi amwita Bwana; amekuwaje mwana wake? Na watu wote walipokuwa wakimsikiliza, aliwaambia wanafunzi wake, Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele karamuni. Wanakula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu. Hao watapata hukumu iliyo kuu.