Yoshua 18:1-7
Yoshua 18:1-7 SRUV
Kisha mkutano mzima wa wana wa Israeli walikutana pamoja hapo Shilo, wakasimamisha hema ya kukutania huko; nayo nchi ilikuwa imeshindwa mbele zao. Yalikuwa yamebaki kati yao makabila saba ya wana wa Israeli ambayo yalikuwa hayajagawiwa urithi wao. Yoshua akawauliza wana wa Israeli, akasema, Je! Hata lini mtakuwa walegevu katika kuingia kwenu na kuimiliki hiyo nchi, ambayo yeye BWANA, Mungu wa baba zenu, amewapa? Haya, jichagulieni watu watatu kwa ajili ya kila kabila; nami nitawatuma, nao watainuka waende kati ya hiyo nchi, na kuiandika kama urithi wao ulivyo; kisha watanijia. Watu hao wataigawanya nchi iwe mafungu saba; Yuda atakaa katika mpaka wake huko upande wa kusini, na nyumba ya Yusufu watakaa katika mpaka wao upande wa kaskazini. Nanyi mtaiandika nchi iwe mafungu saba, kisha hayo maandiko yake mtaniletea mimi hapa; nami nitawapigia kura hapa mbele ya BWANA, Mungu wetu. Kwa maana Walawi hawana fungu kati yenu; Kwa kuwa huo ukuhani wa BWANA ndio urithi wao; tena Gadi, na Reubeni, na hiyo nusu ya kabila la Manase, wamekwisha pata urithi wao ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki, ambao walipewa na Musa, mtumishi wa BWANA.