Yohana 19:31-42
Yohana 19:31-42 SRUV
Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe. Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulubiwa pamoja naye. Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki. Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie, Hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko lingine lanena, Watamtazama yeye waliyemchoma. Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu, (lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake. Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta mchanganyiko wa manemane na uudi, yapata ratili mia. Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika. Na pale pale aliposulubiwa palikuwa na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi jipya, ambalo hajatiwa bado mtu yeyote ndani yake. Humo basi, kwa sababu ya Maandalio ya Wayahudi, wakamweka Yesu; maana lile kaburi lilikuwa karibu.