Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yakobo 5:1-12

Yakobo 5:1-12 SRUV

Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige mayowe kwa sababu ya mateso yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliokosa kuwalipa kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejinenepesha mioyo yenu kama kwa siku ya kuchinjwa. Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi. Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliostahimili. Mmesikia habari za kustahimili kwake Ayubu, kuona mwisho Bwana aliyomtendea, jinsi Bwana alivyo mwingi wa rehema na mwenye huruma. Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali “ndiyo” yenu na iwe ndiyo, na “Hapana” yenu iwe hapana, msije mkaanguka katika hukumu.

Soma Yakobo 5