Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 8:9-22

Isaya 8:9-22 SRUV

Ungameni pamoja, enyi makabila ya watu, Nanyi mtavunjwa vipande vipande; Tegeni masikio, ninyi nyote wa nchi zilizo mbali; Jitahidini, nanyi mtavunjwa vipande vipande; Jitahidini, nanyi mtavunjwa vipande vipande. Fanyeni shauri pamoja, nalo litabatilika; Semeni neno, lakini halitasimama; Kwa maana Mungu yu pamoja nasi. Maana BWANA aliniambia hivi, kwa mkono hodari, akanifundisha nisiende katika njia ya watu hawa, akisema, Msiseme, Ni njama, kuhusu mambo yote ambayo watu hawa watasema, Ni njama; msihofu kwa hofu yao, wala msiogope. BWANA wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu. Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu. Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa. Ufunge huo ushuhuda, ukaitie mhuri sheria kati ya wanafunzi wangu. Nami nitamngojea BWANA, awafichaye uso wake nyumba ya Yakobo, nami nitamtazamia. Angalieni, mimi na watoto hawa niliopewa na BWANA tu ishara na ajabu katika Israeli, zitokazo kwa BWANA wa majeshi, yeye akaaye katika mlima Sayuni. Na wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunong'ona; je! Haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je! Waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai? Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi kulingana na neno hili, bila shaka kwa hao hakuna asubuhi. Nao watapita katikati yake, wamedhikika sana na kuwa na njaa; na itakuwa watakapoona njaa, watalalamika na kuapa kwa mfalme wao, na kwa Mungu wao, na kuelekeza nyuso zao juu; nao wataiangalia nchi, na, tazama, shida na giza; hapatakuwa changamko kwa sababu ya dhiki; nao watafukuzwa na kuingia katika giza kubwa.

Soma Isaya 8