Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 40:12-31

Isaya 40:12-31 SRUV

Ni nani aliyeyapima maji kwa konzi ya mkono wake, na kuzikadiria mbingu kwa shubiri, na kuyashika mavumbi ya dunia katika pishi, na kuipima milima kwa uzani, na vilima kama kwa mizani? Ni nani aliyemwongoza Roho ya BWANA, na kumfundisha kwa kuwa mshauri wake? Alifanya shauri na nani, ni nani aliyemwelimisha na kumfunza njia ya hukumu, na kumfunza maarifa, na kumwonesha njia ya fahamu? Tazama, mataifa ni kama tone la maji katika ndoo, huhesabiwa kuwa kama mavumbi membamba katika mizani; tazama, yeye huvinyanyua visiwa kama ni kitu kidogo sana. Lebanoni nao hautoshelezi kwa kuni, wala wanyama wake hawatoshi kwa kafara. Mataifa yote huwa kama si kitu mbele zake; huhesabiwa kwake kuwa duni kabisa na batili. Basi, mtamlinganisha Mungu na nani? Au mtamfananisha na mfano wa namna gani? Sanamu! Fundi mmoja huiyeyusha, na mfua dhahabu huifunika dhahabu, huifulia mikufu ya fedha. Yeye aliye maskini sana hata hawezi kutoa sadaka ya namna hii, huchagua mti usiooza, hujitafutia fundi stadi wa kusimamisha sanamu ya kuchonga isiyoweza kutikisika. Je! Hamkujua? Hamkusikia? Hamkuambiwa tokea mwanzo? Hamkufahamu tangu kuwekwa misingi ya dunia? Yeye ndiye anayeketi juu ya duara ya dunia, na hao wanaokaa ndani yake huwa kama panzi; yeye ndiye azitandazaye mbingu kama pazia na kuzikunjua kama hema ya kukaliwa; ndiye awatanguaye wakuu, na kuwabatilisha waamuzi wa dunia. Naam, hawakupandwa; hawakutiwa katika ardhi kama mbegu; naam, shina lao halikutia mizizi katika ardhi; tena awapuzia tu, wakanyauka, upepo wa kisulisuli wawaondoa kama mabua makavu. Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye? Asema yeye aliye Mtakatifu. Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake. Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, BWANA asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie? Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, BWANA, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na vijana wanaume wataanguka; bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watakimbia, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.

Soma Isaya 40

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Isaya 40:12-31