Isaya 40:1-17
Isaya 40:1-17 SRUV
Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu, asema Mungu wenu. Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa; kwa kuwa amepokea kwa mkono wa BWANA adhabu maradufu kwa dhambi zake zote. Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya BWANA; Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu. Kila bonde litainuliwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipoinuka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patasawazishwa; Na utukufu wa BWANA utafunuliwa, Na watu wote watauona pamoja; Kwa kuwa kinywa cha BWANA kimenena haya. Sikiliza, ni sauti ya mtu asemaye, Lia! Nikasema, Nilie nini? Watu wote ni majani, Na wema wake wote ni kama ua la shambani; Majani yakauka, ua lanyauka; Kwa sababu pumzi ya BWANA yapita juu yake. Hakika watu ni majani. Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu litasimama milele. Wewe uuhubiriye Sayuni habari njema, Panda juu ya mlima mrefu; Wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema, Paza sauti kwa nguvu; Paza sauti yako, usiogope; Iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu. Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa, Na mkono wake ndio utakaomtawalia; Tazameni, thawabu yake i pamoja naye, Na fidia yake i mbele zake. Atalilisha kundi lake kama mchungaji, Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake; Na kuwachukua kifuani mwake, Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole. Ni nani aliyeyapima maji kwa konzi ya mkono wake, na kuzikadiria mbingu kwa shubiri, na kuyashika mavumbi ya dunia katika pishi, na kuipima milima kwa uzani, na vilima kama kwa mizani? Ni nani aliyemwongoza Roho ya BWANA, na kumfundisha kwa kuwa mshauri wake? Alifanya shauri na nani, ni nani aliyemwelimisha na kumfunza njia ya hukumu, na kumfunza maarifa, na kumwonesha njia ya fahamu? Tazama, mataifa ni kama tone la maji katika ndoo, huhesabiwa kuwa kama mavumbi membamba katika mizani; tazama, yeye huvinyanyua visiwa kama ni kitu kidogo sana. Lebanoni nao hautoshelezi kwa kuni, wala wanyama wake hawatoshi kwa kafara. Mataifa yote huwa kama si kitu mbele zake; huhesabiwa kwake kuwa duni kabisa na batili.