Mwanzo 8:1-14
Mwanzo 8:1-14 SRUV
Na Mungu akamkumbuka Nuhu, na kila kilicho hai, na wanyama wote waliokuwamo pamoja naye katika safina; Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakapungua; chemchemi za vilindi zikafungwa, pia na madirisha ya mbinguni, mvua kutoka mbinguni ikazuiliwa; maji yakadumu kuondoka katika nchi; na mwisho wa siku mia moja na hamsini maji yakapunguka. Mwezi wa saba, siku ya kumi na saba ya mwezi, safina ikatua juu ya milima ya Ararati. Maji yakapungukapunguka hata mwezi wa kumi; mwezi huo wa kumi, siku ya kwanza ya mwezi, vilele vya milima vikaonekana. Ikawa baada ya siku arubaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huku na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi. Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani. Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelichuma, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi. Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe. Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka. Na mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, nchi ilikuwa kavu.