Mwanzo 6:1-8
Mwanzo 6:1-8 SRUV
Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wowote waliowachagua. BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni mwili; basi siku zake zitakuwa miaka mia moja na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu siku zote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemwumba mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. BWANA akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewaumba. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA.