Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 48:1-16

Mwanzo 48:1-16 SRUV

Ikawa, baada ya mambo hayo, Yusufu akaambiwa, Tazama, baba yako ni mgonjwa; akawatwaa wanawe wawili, Manase na Efraimu, pamoja naye. Naye Yakobo akaarifiwa ya kwamba, Angalia, mwanao Yusufu anakuja kwako. Israeli akajitia nguvu, akaketi juu ya kitanda. Yakobo akamwambia Yusufu, Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu, katika nchi ya Kanaani, akanibariki, akaniambia, Mimi hapa, nitakuongezea uzao wako, na kukuzidisha, nami nitakufanya uwe kundi la mataifa; kisha nitawapa wazao wako nchi hii baada yako, iwe milki ya milele. Basi sasa wanao wawili uliozaliwa katika nchi ya Misri kabla sijaja kwako Misri ni watoto wangu, yaani, Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama Reubeni na Simeoni. Na wazao wako utakaozaa baada ya hawa watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao. Na mimi nilipokuja kutoka Padan, Raheli akanifia katika nchi ya Kanaani, njiani, si mwendo mkubwa kabla ya kufika Efrata. Nikamzika katika njia ya Efrata, ndio Bethlehemu. Israeli akawaona wana wa Yusufu, akasema, Ni nani hawa? Yusufu akamwambia babaye, Hawa ni wanangu, Mungu alionipa nikiwa hapa. Akasema, Tafadhali uwalete kwangu nami nitawabariki. Na macho ya Israeli yalikuwa mazito kwa uzee, wala hakuweza kuona vizuri. Akawaleta kwake, naye akawabusu, na kuwakumbatia. Israeli akamwambia Yusufu, Sikudhani ya kwamba nitakuona uso wako, na Mungu amenionesha na uzao wako pia. Yusufu akawatoa katika magoti yake, naye akainama kifudifudi Yusufu akawaweka wote wawili, Efraimu katika mkono wake wa kulia, kuelekea mkono wa kushoto wa Israeli; na Manase katika mkono wake wa kushoto, kuelekea mkono wa kulia wa Israeli, akawasongeza karibu naye. Israeli akanyosha mkono wake wa kulia akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, aliyekuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, huku akijua atiavyo mikono; maana Manase ndiye aliyezaliwa kwanza. Akambariki Yusufu, akasema, Mungu ambaye baba zangu, Abrahamu na Isaka, walienenda mbele zake, yeye Mungu aliyenilisha, maisha yangu yote, hata siku hii ya leo, naye Malaika aliyeniokoa na maovu yote, na awabariki vijana hawa; jina langu na litajwe juu yao, na jina la baba zangu, Abrahamu na Isaka; na wawe wingi wa watu kati ya nchi.

Soma Mwanzo 48