Mwanzo 44:1-17
Mwanzo 44:1-17 SRUV
Akamwamuru yule msimamizi wa nyumba yake akisema, Jaza magunia ya watu hawa chakula kwa kadiri wawezavyo kuchukua, utie na fedha ya kila mtu kinywani mwa gunia lake. Na kikombe changu, kikombe kile cha fedha, ukitie kinywani mwa gunia la yule mdogo pamoja na fedha ya nafaka yake. Akafanya kama vile alivyomwambia Yusufu. Asubuhi kulipopambazuka, hao watu wakapewa ruhusa, wao na punda wao. Na walipotoka mjini, kabla hawajaendelea sana, Yusufu akamwambia yule msimamizi wa nyumba yake, Ondoka, uwafuate watu hawa, nawe utakapowapata, waambie, Kwa nini mmelipa mabaya kwa mema? Je! Kikombe hiki, sicho anyweacho bwana wangu? Naye hufanya uaguzi kwacho. Mmefanya vibaya kwa kufanya hivi. Akawafuata, akawapata, na kuwaambia maneno hayo. Wakamwambia, Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? Hasha! Watumwa wako wasifanye hivi. Tazama, hizo fedha mlizoziona kinywani mwa magunia yetu tumekuletea tena kutoka nchi ya Kanaani. Tuwezeje sisi kuiba nyumbani mwa Bwana wako fedha au dhahabu? Atakayeonekana kuwa nacho miongoni mwa watumwa wako, na afe, na sisi nasi tutakuwa watumwa wa bwana wangu. Akasema, Basi na iwe hivyo kama mlivyosema, Mtu atakayeonekana kuwa nacho atakuwa mtumwa wangu, na ninyi mtakuwa hamna hatia. Wakafanya haraka, wakashusha kila mtu gunia lake, na kufungua kila mtu gunia lake. Naye akatafuta, akaanza kwa mkubwa na kuisha kwa mdogo. Kikombe kikaonekana katika gunia la Benyamini. Wakararua nguo zao, wakaweka kila mtu mzigo wake juu ya punda wake, wakarudi mjini. Akaja Yuda na ndugu zake nyumbani kwa Yusufu, naye mwenyewe alikuwamo, nao wakamwangukia kifudifudi. Yusufu akawaambia, Ni tendo gani hili mlilolitenda? Hamkujua ya kwamba mtu kama mimi naweza kufanya uaguzi? Yuda akasema, Tumwambie nini bwana wangu? Tusemeje! Tujivutieje haki? Mungu ameona uovu wa watumwa wako. Tazama, sisi ni watumwa wa bwana wangu, sisi na yeye ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake. Akasema, Hasha! Nisifanye hivi; mtu ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake, ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Nanyi nendeni zenu kwa amani kwa baba yenu.