Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 41:1-13

Mwanzo 41:1-13 SRUV

Ikawa, baada ya miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto. Na tazama, ng'ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini. Na tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng'ombe wengine ukingoni mwa mto. Kisha hao ng'ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng'ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka. Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema. Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu. Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo. Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo. Farao aliwakasirikia watumishi wake, akanitia nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari walinzi, mimi na mkuu wa waokaji. Tukaota ndoto usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota. Na huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari, tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama ilivyokuwa ndoto yake. Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea; mimi nilirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa.

Soma Mwanzo 41