Mwanzo 35:1-27
Mwanzo 35:1-27 SRUV
Mungu akamwambia Yakobo, Ondoka, panda uende Betheli, ukakae huko; ukamfanyie Mungu madhabahu huko; yeye aliyekutokea ulipomkimbia Esau, ndugu yako. Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu. Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia Mungu madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea. Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na vipuli vilivyokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu. Wakashika njia, hofu ya Mungu ikaishika miji iliyowazunguka, wala hawakuwafuata wana wa Yakobo. Basi Yakobo akafika Luzu, katika nchi ya Kanaani, ndio Betheli, yeye na watu wote waliokuwa pamoja naye. Akajenga huko madhabahu, akapaita mahali pale, El-Betheli; kwa sababu huko Mungu alimtokea, hapo alipomkimbia ndugu yake. Akafa Debora mlezi wa Rebeka, akazikwa chini ya Betheli, chini ya mwaloni; na jina lake likaitwa Alon-bakuthi. Mungu akamtokea Yakobo tena, aliporudi kutoka Padan-aramu akambariki. Mungu akamwambia, Jina lako ni Yakobo; hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli. Mungu akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uzidi ukaongezeke. Taifa na kundi la mataifa watatoka kwako, na wafalme watatoka katika uzao wako. Na nchi hii niliyowapa Abrahamu na Isaka nitakupa wewe, na uzao wako baada yako nitawapa nchi hiyo. Mungu akakwea juu kutoka kwake mahali hapo aliposema naye. Yakobo akasimamisha nguzo mahali aliposema naye, nguzo ya mawe, akamimina juu yake sadaka ya kinywaji, akamimina mafuta juu yake. Yakobo akapaita mahali pale, Mungu aliposema naye, Betheli. Wakasafiri kutoka Betheli, na kabla ya kufika Efrata, Raheli akashikwa na uchungu wa kuzaa, na uchungu wake ulikuwa mkali. Ikawa alipokuwa anashikwa sana na uchungu, mkunga akamwambia, Usiogope, maana sasa utamzaa mwanamume mwingine. Ikawa hapo katika kutoa roho yake, maana alikufa, akamwita jina lake Benoni, lakini babaye alimwita Benyamini. Akafa Raheli, akazikwa katika njia ya Efrata, ndio Bethlehemu. Yakobo akasimamisha nguzo juu ya kaburi lake, ndiyo nguzo ya kaburi la Raheli hata leo. Kisha akasafiri Israeli akapiga hema yake upande wa pili wa mnara wa Ederi. Ikawa Israeli alipokuwa akikaa katika nchi ile, Reubeni akaenda akalala na Bilha, suria wa babaye; Israeli akasikia habari. Basi hao wana wa Yakobo walikuwa kumi na wawili. Wana wa Lea ni Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, na Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Zabuloni. Wana wa Raheli, ni Yusufu na Benyamini. Wana wa Bilha, kijakazi wa Raheli, ni Dani na Naftali. Wana wa Zilpa, kijakazi wa Lea, ni Gadi na Asheri. Hawa ndio wana wa Yakobo aliozaliwa katika Padan-aramu. Yakobo akaja kwa Isaka, babaye, huko Mamre, mji wa Arba, ndio Hebroni, walipokaa ugenini Abrahamu na Isaka.