Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 28:1-16

Mwanzo 28:1-16 SRUV

Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani. Ondoka, uende Padan-aramu, mpaka nyumba ya Bethueli baba ya mama yako, ukajitwalie huko mke katika binti za Labani, ndugu wa mama yako. Na Mungu Mwenyezi, akubariki, akuzidishe, na kukuongeza, ili uwe mtu wa watu wengi. Akupe baraka ya Abrahamu, wewe na uzao wako pamoja nawe, upate kuirithi nchi ya kusafiri kwako, Mungu aliyompa Abrahamu. Basi Isaka akamtuma Yakobo, naye akaenda Padan-aramu, kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mshami, ndugu wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau. Esau akaona ya kwamba Isaka amembariki Yakobo na kumtuma Padan-aramu, ili ajitwalie mke huko, na katika kumbariki akamwagiza, akasema, Usioe mke wa binti za Kanaani, na ya kuwa Yakobo amewatii babaye na mamaye, akaenda Padan-aramu. Esau akaona ya kuwa binti za Kanaani hawakumpendeza Isaka, baba yake. Basi Esau akaenda kwa Ishmaeli akamtwaa Mahalathi, binti Ishmaeli mwana wa Abrahamu, ndugu wa Nebayothi, kuwa mkewe pamoja na wakeze aliokuwa nao. Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Abrahamu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii unayolala nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, ijapokuwa mimi sikujua.

Soma Mwanzo 28