Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 27:1-17

Mwanzo 27:1-17 SRUV

Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia, Mwanangu. Naye akamwitikia, Mimi hapa. Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu. Basi, nakuomba, chukua uta wako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo; ukaniandalie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa. Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda mbugani awinde mawindo, ayalete. Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, akisema, Angalia, nimemsikia baba yako akisema na Esau, ndugu yako, akinena, Niletee mawindo, ukanifanyie chakula kitamu ili nile, na kukubariki mbele za BWANA kabla ya kufa kwangu. Basi, mwanangu, sikiliza sauti yangu kama nitakavyokuagiza. Nenda sasa kundini ukanitwalie wana-mbuzi wawili walio wema, nami nitawafanya chakula kitamu kwa baba yako, namna ile aipendayo. Kisha utampelekea baba yako, apate kula, ili akubariki kabla ya kufa kwake. Yakobo akamwambia Rebeka mamaye, Esau ndugu yangu ni mtu mwenye malaika, na mimi ni mtu laini. Labda baba yangu atanipapasa, nami nitakuwa machoni pake kama mdanganyifu; nami nitaleta juu yangu laana wala si baraka. Mamaye akamwambia, Laana yako na iwe juu yangu, mwanangu, usikie sauti yangu tu, nenda ukaniletee wana-mbuzi. Akaenda, akawatwaa, akamletea mamaye. Mamaye akafanya chakula kitamu namna ile aliyopenda babaye. Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo yake. Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu, na mkate aliouandaa.

Soma Mwanzo 27