Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 24:48-67

Mwanzo 24:48-67 SRUV

Nikainama, nikamsujudia BWANA, nikamtukuza BWANA, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, aliyeniongoza njiani, nimtwalie mwana wa bwana wangu binti wa ndugu yake. Basi, kama mnataka kumfanyia rehema na kweli bwana wangu, niambieni kama sivyo, niambieni; ili nigeuke upande wa kulia au wa kushoto. Ndipo Labani na Bethueli wakajibu wakasema, Neno hili limetoka kwa BWANA, wala sisi hatuwezi kukuambia neno jema wala baya. Tazama, huyo Rebeka yuko mbele yako, umchukue, ukaende zako awe mke wa mwana wa bwana wako, kama alivyosema BWANA. Ikawa mtumishi wa Abrahamu aliposikia maneno yao, akainama hata nchi mbele za BWANA. Kisha huyo mtumishi akatoa vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, akampa Rebeka; na vitu vya thamani akampa nduguye na mamaye pia. Wakala, wakanywa, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, nao wakakaa usiku. Wakaondoka asubuhi, naye akasema, Nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu. Kaka yake na mama yake wakasema, Msichana na akae kwetu kama siku kumi, zisipungue, baadaye aende. Naye akawaambia, Msinikawilishe, mradi BWANA amefanikisha njia yangu; nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu. Wakasema, Na tumwite huyo msichana, tumwulize mwenyewe. Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda. Ndipo wakampeleka Rebeka dada yao, na yaya wake, na mtumishi wa Abrahamu, na watu wake. Wakambariki Rebeka, wakamwambia, Dada yetu, wewe uwe mama wa elfu kumi, mara elfu nyingi, na wazao wako waurithi mlango wa hao wawachukiao. Rebeka akaondoka na vijakazi wake, nao wakapanda juu ya ngamia, wakamfuata yule mtu. Naye huyo mtumishi akamchukua Rebeka akaenda zake. Basi Isaka alikuwa amekuja kwa njia ya Beer-lahai-roi, maana alikaa katika nchi ya kusini. Isaka akatoka ili kutafakari shambani wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja. Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia. Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye shambani kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika. Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda. Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mama yake.

Soma Mwanzo 24

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 24:48-67