Ezekieli 29:15-21
Ezekieli 29:15-21 SRUV
Utakuwa duni kuliko falme zote; wala hautajiinua tena juu ya mataifa; nami nitawapunguza, ili wasitawale tena juu ya mataifa. Wala hautakuwa tena tegemeo la nyumba ya Israeli, kufanya maovu yakumbukwe, watakapogeuka kuangalia nyuma yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU. Ikawa katika mwaka wa ishirini na saba, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, Nebukadneza, mfalme wa Babeli, alilifanyisha jeshi lake kazi ngumu juu ya Tiro; kila kichwa kilitiwa upara, na kila bega liliambuliwa ngozi, lakini hakuna mshahara uliotoka Tiro, sio wake wala wa jeshi lake, kwa kazi ile aliyofanya juu yake. Basi, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitampa Nebukadneza, mfalme wa Babeli, hiyo nchi ya Misri; naye atawachukua watu wake jamii yote pia, na kutwaa mateka yake, na kutwaa mawindo yake, nayo yatakuwa ndio mshahara wa jeshi lake. Nimempa nchi ya Misri kuwa malipo ya kazi aliyofanya, kwa sababu walifanya kazi kwa ajili yangu; asema Bwana MUNGU. Siku ile nitawachipushia nyumba ya Israeli pembe, nami nitakujalia kufumbua kinywa kati yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.