Kutoka 3:1-15
Kutoka 3:1-15 SRUV
Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kichaka; akatazama, na kumbe! Kile kichaka kiliwaka moto, nacho kichaka hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa niende nione kioja hiki, kwa nini kichaka hiki hakiteketei. BWANA alipoona ya kuwa ameenda ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kichaka, akasema, Musa! Musa! Akaitika, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni mahali patakatifu. Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akafunika uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe kutoka kwa mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hadi nchi njema, kisha pana; nchi itiririkayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri. Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu. Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake ni nani? Niwaambie nini? Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO; akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu. Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.