Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 9:26-43

Matendo 9:26-43 SRUV

Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kigiriki. Nao wakajaribu kumwua. Lakini ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakamtuma aende Tarso. Basi kanisa likapata raha kote katika Yudea na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu. Wakati Petro alipokuwa akizungukazunguka pande zote akawateremkia na watakatifu waliokaa Lida. Akamwona mtu mmoja huko, jina lake Ainea, mtu huyo alikuwa amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza. Petro akamwambia, Ainea, Yesu Kristo akuponya; inuka, ujitandikie. Mara akainuka. Na watu wote waliokaa Lida na Sharoni wakamwona, wakamgeukia Bwana. Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; wakati walipokwisha kumwosha, wakamweka ghorofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi waliosikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Njoo kwetu pasipo kukawia. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu ghorofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, inuka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa mkono, akamwinua; hata kisha akawaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, akiwa hai. Ikajulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana. Basi Petro akakaa siku kadhaa huko Yafa, nyumbani mwa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi.

Soma Matendo 9

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Matendo 9:26-43

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha