Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 22:3-21

Matendo 22:3-21 SRUV

Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nilizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihada kubwa kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi; nikawaudhi watu wa Njia hii hata kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake. Kama Kuhani Mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia, ambao nilipokea barua kutoka kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili niwalete wale waliokuwa huko hadi Yerusalemu, wakiwa wamefungwa, ili waadhibiwe. Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafla nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi. Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami. Nikasema, Nifanye nini, Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye. Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski. Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko, Akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, pata kuona tena. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile. Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Basi sasa, mbona unakawia? Simama, ubatizwe, ukaoshwe dhambi zako, ukiliitia jina lake. Ikawa nilipokwisha kurudi Yerusalemu, nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, nikawa katika hali ya kuzimia roho, nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako kuhusu habari zangu. Nami nikasema, Bwana, wanajua hao ya kuwa mimi nilikuwa nikiwafunga gerezani wale wanaokuamini na kuwapiga katika kila sinagogi. Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua. Naye akaniambia, Nenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa.

Soma Matendo 22

Video ya Matendo 22:3-21

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Matendo 22:3-21