Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 20:1-16

Matendo 20:1-16 SRUV

Ghasia ile ilipokoma, Paulo akatuma kuwaita wanafunzi akawaonya, akaagana nao, kisha akaondoka aende zake mpaka Makedonia. Naye akiisha kupita pande zile na kuwafariji kwa maneno mengi, akafika Ugiriki. Alipokwisha kukaa huko miezi mitatu, na Wayahudi kumfanyia vitimvi, alipotaka kwenda Shamu kwa njia ya bahari; basi akaazimu kurejea kwa njia ya Makedonia. Watu hawa wakafuatana naye, Sopatro Mberea, mwana wa Piro, na Aristarko na Sekundo, watu wa Thesalonike; na Gayo mtu wa Derbe, na Timotheo; na Tikiko na Trofimo watu wa Asia. Ila watu hao wamekwisha kutangulia wakamngojea Troa. Sisi tukatweka baada ya siku za mikate isiyotiwa chachu, tukatoka Filipi, tukawafikia Troa, baada ya safari ya siku tano, tukakaa huko siku saba. Siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubia, maana aliazimia kusafiri siku iliyofuata, naye akafululiza maneno yake hadi usiku wa manane. Palikuwa na taa nyingi katika ghorofa lile tulipokuwa tumekusanyika. Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka ghorofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa. Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake. Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hadi alfajiri, ndipo akaenda zake. Wakamleta yule kijana, akiwa mzima, wakafarijika faraja kubwa sana. Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimia kwenda kwa miguu. Alipotufikia huko Aso, tukampakia, kisha tukafika Mitilene. Tukatweka kutoka huko, na siku ya pili tukafika mahali panapokabili Kio; siku ya tatu tukawasili Samo, tukakaa Trogilio, siku ya nne tukafika Mileto. Kwa sababu Paulo alikusudia kusafiri pasipo kupitia Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana.

Soma Matendo 20

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Matendo 20:1-16