Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 2:1-13

Matendo 2:1-13 SRUV

Wakati ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafla toka mbinguni sauti kama mvumo wa upepo mkali ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Yudea na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu. Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya? Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya.

Soma Matendo 2