Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 18:19-33

2 Samweli 18:19-33 SRUV

Basi Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akasema, Niende mbio sasa, nikampelekee mfalme habari, jinsi BWANA alivyomlipiza kisasi juu ya adui zake. Yoabu akamwambia, Wewe hutakuwa mchukua habari leo, siku nyingine utachukua habari; lakini leo hutachukua habari, kwa sababu mwana wa mfalme amekufa. Ndipo Yoabu akamwambia Mkushi mmoja, Nenda ukamwambie mfalme hayo uliyoyaona. Na huyo Mkushi akajiinamisha mbele ya Yoabu, akaenda zake mbio. Ndipo Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akamwambia Yoabu mara ya pili, Haidhuru, tafadhali nipe ruhusa, nipige mbio na mimi nyuma ya huyo Mkushi. Naye Yoabu akasema, Mbona wewe unataka kupiga mbio, mwanangu, hali hutapata kitu kwa habari hizo unazopeleka? Akasema, Haidhuru, nitapiga mbio. Akamwambia, Haya, piga mbio. Ndipo Ahimaasi akapiga mbio, akishika njia ya uwandani, akampita yule Mkushi. Basi Daudi alikuwa ameketi kati ya malango mawili; mlinzi akapanda juu hata dari ya lile lango hata ukutani, akainua macho yake, akaangalia, na tazama, mtu anakuja mbio peke yake. Mlinzi akapaaza sauti, akamwambia mfalme. Naye mfalme akasema, Kama yuko peke yake, ana habari kinywani mwake. Akaja mbio, akakaribia. Kisha huyo mlinzi akaona mtu mwingine anapiga mbio; mlinzi akamwita bawabu, akasema, Angalia, mtu mwingine anakuja mbio peke yake. Mfalme akasema, Huyu naye analeta habari. Na huyo mlinzi akasema, Nionavyo mimi, kupiga mbio kwake yule wa kwanza ni kama kupiga mbio kwake Ahimaasi, mwana wa Sadoki. Naye mfalme akasema, Yeye ni mtu mwema, anakuja na habari njema. Ahimaasi akainua sauti yake, akamwambia mfalme, Amani. Akainama mbele ya mfalme kifudifudi, akasema, Ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyewatoa watu hao walioiinua mikono yao juu ya bwana wangu, mfalme. Mfalme akauliza, Je! Yule kijana, Absalomu, yuko salama? Ahimaasi akajibu, Yoabu aliponituma mimi mtumishi wa mfalme, mimi mtumishi wako, niliona kishindo kikubwa, lakini sikujua sababu yake. Naye mfalme akasema, Geuka, usimame hapa. Akageuka, akasimama. Na tazama, yule Mkushi akafika; Mkushi akasema, Nina habari kwa bwana wangu mfalme; kwa maana BWANA amekulipizia kisasi leo juu ya hao wote walioinuka kupigana nawe. Naye mfalme akamwambia yule Mkushi, Yule kijana, Absalomu, je! Yuko salama? Yule Mkushi akajibu, Adui za bwana wangu mfalme, na wote wainukao ili kukudhuru, na wawe kama alivyo yule kijana. Naye mfalme akataabika sana, akapanda juu, akaingia kile chumba kilichokuwa juu ya lango, akalia; na katika kwenda kwake alisema hivi, Mwanangu Absalomu! Ee mwanangu! Mwanangu Absalomu! Laiti ningalikufa badala yako, Absalomu, mwanangu, mwanangu!

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 2 Samweli 18:19-33