Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 10:1-19

2 Samweli 10:1-19 SRUV

Ikawa baadaye, mfalme wa Waamoni akafa, mwanawe Hanuni, akawa mfalme, badala yake. Naye Daudi akasema, Nitamtendea wema Hanuni, mwana wa Nahasi, kama babaye alivyonitendea wema mimi. Basi Daudi akatuma kwa mkono wa watumishi wake, ili kumtuliza kwa habari za babaye. Wakaja watumishi wa Daudi katika nchi ya Waamoni. Lakini wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni, bwana wao, Je! Waona ya kuwa Daudi amemheshimu babayo kwa kutuma kwako wafariji? Je! Daudi hakuwapeleka watumishi wake kwako ili kuuangalia mji, na kuupeleleza, na kuuangamiza? Basi Hanuni akawatwaa hao watumishi wa Daudi, akawanyoa nusu ya ndevu zao, akawakatia nguo zao katikati, hata matakoni, akawatoa waende zao. Watu walipomwambia Daudi habari hizo, akatuma watu kuwalaki; kwa sababu watu hao walikuwa wameaibika sana. Mfalme akasema, Ngojeni Yeriko, hata mtakapoota ndevu zenu, ndipo mrudi. Na Waamoni walipoona ya kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, Waamoni wakatuma na kuwaajiri Washami wa Bethrehobu, na Washami wa Soba, askari elfu ishirini, na mfalme wa Maaka mwenye watu elfu moja, na watu wa Tobu watu elfu kumi na mbili. Naye Daudi aliposikia akamtuma Yoabu, na jeshi lote la mashujaa. Waamoni wakatoka, wakapanga vita mahali pa kuingilia lango; na Washami wa Soba, na wa Rehobu, na watu wa Tobu, na wa Maaka, walikuwa peke yao uwandani. Basi Yoabu alipoona ya kwamba uso wa vita umekuwa juu yake mbele na nyuma, akachagua baadhi ya wateule wote wa Israeli, akawapanga juu ya Washami; akawatia nguvu watu waliosalia mkononi mwa Abishai, nduguye, akawapanga juu ya Waamoni. Akasema, Wakiwa Washami hodari mno kwangu, ndipo wewe utanisaidia, lakini Waamoni wakiwa ni hodari mno kwako, ndipo mimi nitakuja nikusaidie wewe. Uwe hodari, tuwe na ujasiri, kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye BWANA afanye yaliyo mema machoni pake. Basi Yoabu na watu waliokuwa pamoja naye wakakaribia kupigana na Washami; nao wakakimbia mbele yake. Na wana wa Amoni walipoona ya kwamba Washami wamekimbia, wakakimbia nao mbele ya Abishai, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akarudi kutoka kwa wana wa Amoni, akaja Yerusalemu. Na Washami walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, wakakusanyika. Naye Hadadezeri akatuma na kuwaleta Washami waliokuwako ng'ambo ya Mto; nao wakaja Helamu, naye Shobaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri, akawaongoza. Daudi alipoambiwa, akakusanya Israeli wote, akavuka Yordani, akaja Helamu. Nao Washami wakajipanga kinyume cha Daudi, wakapigana naye. Wakakimbia Washami mbele ya Israeli; naye Daudi akawaua katika Washami, watu wa magari mia saba, na wapanda farasi elfu arubaini, naye akampiga huyo Shobaki, jemadari wa jeshi lao, hata akafa huko. Na wafalme wote waliomtumikia Hadadezeri walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, walifanya amani na Israeli, wakawatumikia. Basi Washami wakaogopa kuwasaidia Waamoni tena.