1 Samweli 19:9-24
1 Samweli 19:9-24 SRUV
Tena ikawa, roho mbaya kutoka kwa BWANA ilimjia Sauli, hapo alipoketi ndani ya nyumba yake, akiwa na mkuki wake mkononi mwake; naye Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake. Sauli akajaribu kumpiga Daudi hadi ukutani kwa mkuki wake, ila yeye akaponyoka kutoka mbele ya Sauli, nao huo mkuki akaupiga ukutani; naye Daudi akakimbia, akaokoka usiku ule. Kisha Sauli akatuma wajumbe mpaka nyumbani kwa Daudi, ili wamvizie na kumwua asubuhi; naye Mikali, mkewe Daudi, akamwambia, akasema, Wewe usipojiponya nafsi yako usiku huu, kesho utauawa. Basi Mikali akamteremsha Daudi dirishani; naye akaenda akakimbia na kuokoka. Ndipo Mikali akakitwaa kinyago, na kukilaza kitandani, akatia na mto wa singa za mbuzi kichwani pake, na kukifunika kwa nguo. Naye Sauli alipotuma wajumbe ili kumkamata Daudi, yeye alisema, Mgonjwa. Basi Sauli akawatuma hao wajumbe ili wamtazame Daudi, akisema, Mleteni kwangu juu ya kitanda chake, nipate kumwua. Nao wajumbe walipoingia, kumbe! Kuna kinyago kitandani, na mto wa singa za mbuzi kichwani pake! Sauli akamwambia Mikali, Mbona wewe umenidanganya hivi, na kumwacha adui yangu aende, hata ameniponyoka? Naye Mikali akamjibu Sauli, Yeye aliniambia, Niache niende zangu; kwa nini nikuue? Hivyo Daudi akakimbia, akajiponya, akamwendea Samweli huko Rama, akamwambia hayo yote Sauli aliyomtenda. Kisha yeye na Samweli wakaenda na kukaa katika Nayothi. Naye Sauli akaambiwa, Angalia, yule Daudi yuko katika Nayothi, huko Rama. Basi Sauli akatuma wajumbe ili kumkamata Daudi; nao hapo walipowaona jamaa ya manabii wakitabiri, na Samweli amesimama kama mkuu wao, Roho ya Mungu ikawajia wajumbe wa Sauli, nao pia wakatabiri. Naye Sauli alipoambiwa, alituma wajumbe wengine, wao nao wakatabiri. Naye Sauli akatuma wajumbe tena mara ya tatu, na wao pia wakatabiri. Kisha yeye mwenyewe akaenda Rama, akafika kwenye kile kisima kikubwa kilicho huko Seku; akauliza, akasema, Je! Wako wapi Samweli na Daudi? Na mtu mmoja akajibu, Tazama, wako Nayothi, huko Rama. Basi akaenda Nayothi huko Rama, na Roho ya Mungu ikamjia yeye naye, akaendelea mbele, huku anatabiri, mpaka kufika Nayothi huko Rama. Naye akavua nguo zake, akatabiri mbele ya Samweli, akalala uchi mchana kutwa na usiku kucha siku ile. Kwa hiyo watu wakasema, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?