Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 8:41-53

1 Wafalme 8:41-53 SRUV

Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako; (maana watasikia habari za jina lako kuu, na za mkono wako ulio hodari, na za mkono wako ulionyoshwa); atakapokuja na kuomba kuielekea nyumba hii; basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukatende kwa kadiri ya yote atakayokuomba mgeni huyo; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe kama watu wako Israeli, nao wajue ya kuwa nyumba hii, niliyoijenga, imeitwa kwa jina lako. Ikiwa watu wako watoka kwenda kupigana na adui zao, kwa njia yoyote utakayowapeleka, wakikuomba, BWANA, kuuelekea mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako; basi, uyasikie huko mbinguni maombi yao na dua yao, ukaitetee haki yao. Ikiwa wamekutenda dhambi, (maana hakuna mtu asiyetenda dhambi), hata ukawaghadhibikia, ukawatia katika mikono ya adui zao, wawachukue mateka mpaka nchi ya adui zao, iliyo mbali au iliyo karibu; basi, wakijirudia nafsi zao katika nchi ile watakayochukuliwa mateka, wakitubu, na kukusihi katika nchi ya hao waliowachukua mateka, wakisema, Tumekosa, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu; watakaporejea kwako kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya adui zao, waliowachukua mateka, wakikuomba, kwa kuikabili nchi yao, uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako; basi, uyasikie maombi yao na dua yao, huko mbinguni, makao yako, ukaitetee haki yao; ukawasamehe watu wako waliokutenda dhambi, na makosa yao yote waliyokukosa; ukawape kuonewa huruma mbele yao waliowachukua mateka, ili wapate kuwahurumia. Kwa kuwa ni watu wako, na urithi wako, uliowatoa katika Misri, toka katikati ya tanuri ya chuma. Macho yako na yafumbuke, na kuielekea dua ya mtumwa wako, na dua za watu wako Israeli, ukawasikilize kila wakati watakapokulilia. Kwa maana uliwatenga na watu wote wa dunia, wawe urithi wako, kama ulivyonena kwa mdomo wa Musa, mtumishi wako, hapo ulipowatoa baba zetu katika Misri, Ee Bwana MUNGU.