Mit 8:22-36
Mit 8:22-36 SUV
BWANA alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale. Nalitukuka tokea milele, tangu awali, Kabla haijawako dunia. Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, Wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji. Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nalizaliwa. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde Wala chanzo cha mavumbi ya dunia; Alipozithibitisha mbingu nalikuwako; Alipopiga duara katika uso wa bahari; Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari zilipopata nguvu; Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza misingi ya nchi; Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake; Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu. Basi, wanangu, nisikilizeni sasa; Maana heri hao wazishikao amri zangu. Sikieni mafundisho, mpate hekima, Wala msiikatae. Ana heri mtu yule anisikilizaye, Akisubiri sikuzote malangoni pangu, Akingoja penye vizingiti vya milango yangu. Maana yeye anionaye mimi aona uzima, Naye atapata kibali kwa BWANA. Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, Na wao wanichukiao hupenda mauti.