Mit 11:15-31
Mit 11:15-31 SUV
Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia; Achukiaye mambo ya dhamana yu salama. Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; Na watu wakali hushika mali siku zote. Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake. Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika. Haki huelekea uzima; Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe. Wenye kuhalifu moyoni ni chukizo kwa BWANA; Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza. Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu; Bali wazao wa wenye haki wataokoka. Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, Kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili. Haja ya mwenye haki ni mema tu; Bali kutaraji kwake mtu mwovu ni ghadhabu. Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji. Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe. Awanyimaye watu nafaka, watu watamlaani; Auzaye nafaka, baraka itakuwa kichwani pake. Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhili; Atafutaye madhara, hayo yatamjia. Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani. Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili. Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima; Na mwenye hekima huvuta roho za watu. Tazama, mwenye haki atalipwa duniani; Basi mwovu na mkosaji si mara nyingi zaidi?