Mt 27:1-31
Mt 27:1-31 SUV
Na ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu, wapate kumwua; wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato aliyekuwa liwali. Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia. Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe. Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga. Wakuu wa makuhani wakavitwaa vile vipande vya fedha, wakasema, Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka, kwa kuwa ni kima cha damu. Wakafanya shauri, wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni. Kwa hiyo konde lile huitwa konde la damu hata leo. Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Wakavitwaa vipande thelathini vya fedha, kima chake aliyetiwa kima, ambaye baadhi ya Waisraeli walimtia kima; wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza. Naye Yesu akasimama mbele ya liwali; liwali akamwuliza, akasema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Yesu akamwambia, Wewe wasema. Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno. Ndipo Pilato akamwambia, Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia? Asimjibu hata neno moja, hata liwali akastaajabu sana. Basi wakati wa siku kuu, liwali desturi yake huwafungulia mkutano mfungwa mmoja waliyemtaka. Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba. Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda. Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake. Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu. Basi liwali akajibu, akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi katika hawa wawili? Wakasema, Baraba. Pilato akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulibiwe. Akasema, Kwani? Ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, wakisema, Na asulibiwe. Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe. Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu. Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe. Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha.