Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Lk 15:1-10

Lk 15:1-10 SUV

Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao. Akawaambia mfano huu, akisema, Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone? Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi. Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea. Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu. Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione? Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea. Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.