Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Lk 12:35-48

Lk 12:35-48 SUV

Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao. Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu. Petro akamwambia, Bwana, mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia? Bwana akasema, Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo. Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini. Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.