Yer 48
48
Hukumu ya Moabu
1 #
Isa 15:1; Hes 32:38 Habari za Moabu. BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ole wake Nebo! Kwa maana umeharibika; Kiriathaimu umeaibishwa, umetwaliwa; Misgabu umeaibishwa, nao umebomolewa. 2Sifa za Moabu haziko tena; katika Heshboni wameazimia mabaya juu yake, Haya! Njoni, na tumkatilie mbali asiwe taifa. Wewe nawe, Ee Madmena, utanyamazishwa; upanga utakufuatia.
3Sauti ya kilio toka Horonaimu,
Ya kutekwa na uharibifu mkuu.
4Moabu umeharibika;
Wadogo wake wamewasikiza watu kilio.
5Kwa maana watu wapandapo huko Luhithi
Watapanda wasiache kulia;
Nao watu watelemkapo huko Horonaimu
Wameisikia huzuni ya kilio cha uharibifu.
6Haya! Kimbieni! Jiokoeni nafsi zenu!
Mkawe kama mtu aliye mkiwa.
7 #
Zab 49:6,7; 52:7; Yer 9:23; 1 Tim 6:17; Ufu 18:17; Hes 21:29 Maana, kwa kuwa umeyatumainia matendo yako, na hazina zako, wewe nawe utatwaliwa; na Kemoshi atatoka aende katika uhamisho, makuhani wake na wakuu wake pamoja. 8Naye mwenye kuteka nyara atakuja juu ya kila mji, wala hapana mji utakaookoka; bonde nalo litaangamia, nayo nchi tambarare itaharibiwa; kama BWANA alivyosema. 9Mpe Moabu mabawa, apate kuruka na kwenda zake; na miji yake itakuwa ukiwa, isiwe na mtu wa kukaa ndani yake. 10#1 Sam 15:3Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya BWANA kwa ulegevu; na alaaniwe auzuiaye upanga wake usimwage damu. 11#Sef 1:12Moabu amestarehe tangu ujana wake, naye ametulia juu ya sira zake, wala hakumiminwa kutoka chombo kimoja kutiwa chombo kingine, wala hakwenda kufungwa; kwa hiyo ladha yake anakaa nayo, wala harufu yake haikubadilika. 12Basi, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, ambazo nitampelekea wamiminao, nao watammimina, nao watamwaga vyote vilivyomo vyomboni mwake, na kuzivunja chupa zake vipande vipande. 13#Amu 11:24; Hos 10:6; 1 Fal 12:29; Amo 5:5,6Na Moabu ataona haya kwa ajili ya Kemoshi, kama nyumba ya Israeli ilivyoona haya kwa ajili ya Betheli, matumaini yao. 14#Zab 33:6; Mhu 9:11; Isa 16:6; Yer 9:23Mwasemaje ninyi, Sisi tu mashujaa, watu hodari wa vita. 15#Yer 50:27; 51:57; Mal 1:14Moabu ameharibika, na moshi wa miji yake umepanda; na vijana wake wateule wametelemka kwenda kuchinjwa, asema Mfalme, ambaye jina lake ni BWANA wa majeshi.
16Msiba wa Moabu umefika karibu,
Na mateso yake yanafanya haraka.
17 #
Isa 9:4; 14:4 Ninyi nyote mnaomzunguka, mlilieni,
Nanyi nyote mlijuao jina lake, semeni,
Jinsi ilivyovunjika fimbo ya enzi,
Fimbo ile iliyokuwa nzuri!
18 #
Isa 47:1; 15:2; Yer 46:19; Hes 21:30 Ee binti ukaaye Diboni,
Shuka toka utukufu wako, ukae katika kiu;
Maana atekaye Moabu amepanda juu yako,
Ameziharibu ngome zako.
19 #
Kum 2:36; 1 Sam 4:13,16 Wewe ukaaye Aroeri,
Simama kando ya njia upeleleze;
Mwulize mwanamume akimbiaye na mwanamke atorokaye,
Sema, Imetendeka nini?
20 #
Hes 21:13
Moabu ameaibishwa, kwa maana amevunjika;
Pigeni yowe na kulia;
Tangazeni habari hii katika Arnoni,
Ya kuwa Moabu ameharibika.
21Na hukumu imeifikilia nchi tambarare; juu ya Holoni, na juu ya Yasa, na juu ya Mefaathi; 22na juu ya Diboni, na juu ya Nebo, na juu ya Beth-diblathaimu; 23na juu ya Kiriathaimu, na juu ya Beth-gamuli, na juu ya Beth-meoni; 24#Amo 2:2na juu ya Keriothi, na juu ya Bozra, na juu ya miji yote ya nchi ya Moabu, iliyo mbali na iliyo karibu. 25Pembe ya Moabu imekatika, na mkono wake umevunjika, asema BWANA. Mlevyeni; kwa maana alijitukuza juu ya BWANA 26#Yer 25:15na Moabu atagaa-gaa katika matapiko yake, naye atadhihakiwa. Kwa maana Israeli, je! Hakuwa dhihaka kwako? 27#Mit 24:17; Sef 2:8; Yer 2:26Alionekana kati ya wevi? Maana kila umtajapo watikisa kichwa chako.
28 #
Zab 55:6,7; Wim 2:14 Enyi mkaao Moabu, iacheni miji,
Enendeni kukaa majabalini;
Mkawe kama njiwa afanyaye kioto chake
Katika ubavu wa mdomo wa shimo.
29 #
Isa 16:6
Tumesikia habari za kiburi cha Moabu;
Ya kuwa ana kiburi kingi;
Jeuri yake, na kiburi chake, na majivuno yake,
Na jinsi alivyotakabari moyoni mwake.
30Najua ghadhabu yake, asema BWANA, ya kuwa si kitu; majisifu yake hayakutenda neno lo lote. 31#Isa 15:5Kwa sababu hiyo nitampigia yowe Moabu, naam, nitapiga kelele kwa ajili ya Moabu yote; nitawaombolezea watu wa Kir-heresi. 32#Hes 21:13Nitakulilia, Ee mzabibu wa Sibma, kwa vilio vipitavyo vilio vya Yazeri; matawi yako yalipita juu ya bahari, yalifika hata bahari ya Yazeri; atekaye nyara ameyaangukia matunda yako ya wakati wa jua, na mavuno yako ya zabibu. 33#Isa 16:9,10; Yoe 1:12Furaha na shangwe zimeondoshwa, katika shamba lizaalo sana, na katika nchi ya Moabu; nami nimeikomesha divai katika mashinikizo; hapana mtu atakayekanyaga zabibu kwa shangwe; shangwe ile itakuwa si shangwe. 34#Isa 15:4-6Toka kilio cha Heshboni mpaka Eleale, naam, mpaka Yahasa, wametoa sauti zao, toka Soari mpaka Horonaimu, hata Eglath-shelishia; maana maji ya Nimrimu nayo yatakuwa ukiwa. 35#Isa 15:2Pamoja na hayo, asema BWANA, nitamkomesha katika Moabu mtu atoaye sadaka katika mahali pa juu, naye awafukiziaye uvumba miungu yake. 36#Mit 11:4; Mhu 5:13,14; Isa 15:7; Lk 12:20,21Kwa sababu hiyo moyo wangu watoa sauti kama filimbi kwa ajili ya Moabu, na kwa ajili ya watu wa Kir-heresi, moyo wangu watoa sauti kama filimbi; kwa kuwa wingi aliojipatia umepotea. 37#Yer 47:5; Mwa 37:34Maana kila kichwa kina upaa, na ndevu zote zimenyolewa; mikono yote ina alama za chale, na viuno vyote vimevikwa nguo za magunia. 38#Yer 22:28Juu ya dari zote za nyumba za Moabu, na katika njia kuu zake, pana maombolezo, kila mahali; kwa maana nimevunja Moabu kama chombo kisichopendeza, asema BWANA. 39Jinsi alivyovunjika! Pigeni yowe! Jinsi Moabu alivyogeuza kisogo kwa haya! Hivyo ndivyo Moabu atakavyokuwa dhihaka, na sababu ya kuwashangaza watu wote wamzungukao.
40 #
Yer 49:22; Dan 7:4; Hos 8:1; Hab 1:8; Isa 8:8 Maana BWANA asema hivi, Tazama, ataruka kama tai, na kutandaza mabawa yake juu ya Moabu. 41#Isa 13:8; Yer 30:6; Mik 4:9Miji imetwaliwa, ngome zimeshambuliwa, na mioyo ya mashujaa wa Moabu siku hiyo itakuwa kama moyo wa mwanamke katika utungu wake. 42#Zab 83:4; Isa 16:13,14; Mit 16:18Na Moabu ataangamizwa, asiwe taifa tena, kwa sababu alijitukuza juu ya BWANA. 43#Isa 24:17,18Hofu, na shimo, na mtego, zaja juu yako, Ee mwenyeji wa Moabu, asema BWANA. 44#Yer 11:23Aikimbiaye hofu ataanguka shimoni; na yeye atokaye shimoni atanaswa kwa mtego; maana nitaleta juu yake, yaani, juu ya Moabu, mwaka wa kujiliwa kwake, asema BWANA.
45 #
Hes 21:28; 24:17 Wamekimbia, wasio na nguvu
Wanasimama chini ya kivuli cha Heshboni;
Ila moto umetoka katika Heshboni,
Na mwali wa moto toka kati ya Sihoni
Nao umekula pembe ya Moabu,
Na utosi wa kichwa wa watu wapigao kelele.
46 #
Hes 21:29; Amu 11:24 Ole wako! Ee Moabu,
Watu wa Kemoshi wamepotea;
Maana wana wako wamechukuliwa mateka,
Na binti zako wamekwenda utumwani.
47 #
Yer 49:6,39 Lakini nitawarudisha watu wa Moabu walio utumwani, siku za mwisho, asema BWANA. Hukumu ya Moabu imefikilia hapa.
Iliyochaguliwa sasa
Yer 48: SUV
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.