Amu 14
14
Ndoa ya Samsoni
1 #
Mwa 38:13; Yos 15:10; Mwa 34:2; Zab 119:37 Samsoni akatelemkia Timna, akaona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti. 2#Mwa 21:21; 34:4Kisha akapanda, akawaambia baba yake na mama yake, akasema, Nimemwona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti; basi mnipatie, nimwoe. 3#Mwa 24:3,4; Kut 34:16; Kum 7:3Ndipo baba yake na mama yake wakamwambia, Je! Hapana mwanamke hata mmoja katika ndugu zako, au katika jamaa zangu zote, hata uende kumwoa mwanamke kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa? Samsoni akamwambia baba yake; Mnipatie huyo, kwa maana ananipendeza sana. 4#Yos 11:20; 2 Nya 10:15Lakini baba yake na mama yake hawakujua ya kuwa jambo hili ni la BWANA; maana alitaka kisa juu ya Wafilisti. Basi wakati ule Wafilisti walikuwa wakiwatawala Israeli.
5Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia. 6#Amu 3:10; 13:25; 1 Sam 11:6Roho ya BWANA ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya. 7Basi akatelemka na kuzungumza na huyo mwanamke; naye akampendeza Samsoni sana. 8Kisha baadaye akarudi ili kumtwaa, naye akageuka kando kuuangalia mzoga wa huyo simba; na tazama, nyuki wengi walikuwamo ndani ya mzoga wa simba, na asali. 9Akatwaa asali mikononi mwake akaenda mbele, huku akila alipokuwa akienenda, akawafikilia babaye na mamaye, akawapa, nao wakala; lakini hakuwaambia ya kuwa ameitwaa hiyo asali katika mzoga wa simba. 10Basi babaye akamtelemkia huyo mwanamke; Samsoni naye akafanya karamu huko; kwa kuwa vijana ndivyo walivyokuwa wakifanya. 11Basi ikawa hapo walipomwona, wakamletea wenziwe thelathini, wawe pamoja naye. 12#1 Fal 10:1; Eze 17:2; Lk 14:7; Mwa 29:27; 45:22; 2 Fal 5:22Samsoni akawaambia, Mimi nitawategea ninyi kitendawili; kama mwaweza kunionyesha katika hizo siku saba za karamu, na kukitambua, ndipo hapo nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavao mengine thelathini; 13lakini msipoweza kunionyesha ndipo hapo ninyi mtanipa mimi mavazi thelathini ya kitani na mavao mengine thelathini. Basi wakamwambia, Haya, tega kitendawili chako, ili tupate kukisikia. 14Naye akawaambia,
Katika huyo mwenye kula kikatoka chakula,
Katika huyo mwenye nguvu ukatoka utamu.
Nao katika siku tatu hawakuweza kukifungua hicho kitendawili. 15#Mwa 3:6; Amu 16:5; Mit 6:26; Mik 7:6; Amu 15:6Ikawa kwa siku ya saba, wakamwambia mkewe Samsoni, Mbembeleze mumeo, ili atuonyeshe hicho kitendawili, tusije tukakuteketeza moto wewe na nyumba ya baba yako; je! Mmetuita ili mpate kuichukua mali yetu? Je! Sivyo? 16#Amu 16:15Basi mkewe Samsoni akalia mbele yake, akasema, Wewe wanichukia tu, wala hunipendi; wewe umewategea kitendawili hao wana wa watu wangu, nawe hukuniambia mimi. Naye akamwambia, Angalia, sikumwambia baba yangu wala mama yangu, nami nikuambie wewe? 17Naye akalia mbele yake hizo siku saba, wakati ulioendelea karamu yao; basi ikawa siku ya saba akamwambia, kwa sababu alikuwa akimsisitiza sana; naye akawaambia wale wana wa watu wake hicho kitendawili. 18Nao watu wa mji wakamwambia siku ya saba kabla ya jua kuchwa,
Ni kitu gani kilicho tamu kuliko asali?
Ni kitu gani kilicho na nguvu kuliko simba?
Naye akawaambia,
Kwamba hamkulima na mtamba wangu,
Hamngekitambua kitendawili changu.
19 #
Hes 11:17; 27:18; Amu 3:10; 13:25; 1 Sam 10:6; 11:6; 16:13; 1 Kor 12:4,11 Roho ya BWANA ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo. Hasira zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake. 20#Amu 15:2; Yn 3:29Lakini huyo mke wa Samsoni aliozwa mwenzake, ambaye alikuwa amemtendea kama rafikiye.
Iliyochaguliwa sasa
Amu 14: SUV
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.