Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isa 40:12-31

Isa 40:12-31 SUV

Ni nani aliyeyapima maji kwa konzi ya mkono wake, na kuzikadiri mbingu kwa shubiri, na kuyashika mavumbi ya dunia katika pishi, na kuipima milima kwa uzani, na vilima kama kwa mizani? Ni nani aliyemwongoza roho ya BWANA, na kumfundisha kwa kuwa mshauri wake? Alifanya shauri na nani, ni nani aliyemwelimisha na kumfunza njia ya hukumu, na kumfunza maarifa, na kumwonyesha njia ya fahamu? Tazama, mataifa ni kama tone la maji katika ndoo, huhesabiwa kuwa kama mavumbi membamba katika mizani; tazama, yeye huvinyanyua visiwa kama ni kitu kidogo sana. Lebanoni nayo hautoshi kwa kuni, wala wanyama wake hawatoshi kwa kafara. Mataifa yote huwa kama si kitu mbele zake; huhesabiwa kwake kuwa duni ya si kitu, na ubatili. Basi, mtamlinganisha Mungu na nani? Au mtamfananisha na mfano wa namna gani? Sanamu fundi mmoja huiyeyusha, na mfua dhahabu huifunika dhahabu, huifulia mikufu ya fedha. Yeye aliye maskini sana hata hawezi kutoa sadaka ya namna hii, huchagua mti usiooza, hujitafutia fundi mstadi wa kusimamisha sanamu ya kuchonga isiyoweza kutikisika. Je! Hamkujua? Hamkusikia? Hamkuambiwa tokea mwanzo? Hamkufahamu tangu kuwekwa misingi ya dunia? Yeye ndiye anayeketi juu ya duara ya dunia, na hao wanaokaa ndani yake huwa kama panzi; yeye ndiye azitandazaye mbingu kama pazia na kuzikunjua kama hema ya kukaliwa; ndiye awatanguaye wakuu, na kuwabatilisha waamuzi wa dunia. Naam, hawakupandwa; hawakutiwa katika ardhi kama mbegu; naam, shina lao halikutia mizizi katika ardhi; tena awapuzia tu, wakanyauka, upepo wa kisulisuli wawaondoa kama mabua makavu. Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye? Asema yeye aliye Mtakatifu. Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake. Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, BWANA asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie? Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, BWANA, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.

Soma Isa 40

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Isa 40:12-31