Mwa 33:12-20
Mwa 33:12-20 SUV
Kisha Esau akamwambia, Twende zetu, tusafiri, nami nitakutangulia. Akamjibu, Bwana wangu anajua ya kuwa watoto ni wachanga, tena kondoo na ng’ombe nilio nao wanyonyesha. Hao wanyama wakiharakishwa siku moja, watakufa wote. Tafadhali bwana wangu na apite mbele ya mtumwa wake; nami nitawaongoza polepole kwa kadiri ya mwendo wa wanyama walio mbele yangu, na kwa kadiri ya mwendo wa watoto, hata nitakapofika kwa bwana wangu huko Seiri. Esau akasema, Nikuachie, basi, baadhi ya watu walio pamoja nami. Akasema, Pana haja gani? Na nione kibali tu machoni pa bwana wangu. Basi Esau akarudi siku ile ile akishika njia yake mpaka Seiri. Yakobo akaendelea mpaka Sukothi. Akajijengea nyumba, akawafanyia makundi yake vibanda. Kwa hiyo jina la mahali pale pakaitwa Sukothi. Yakobo akaja kwa amani mpaka mji wa Shekemu, ulio katika nchi ya Kanaani, alipokuja kutoka Padan-aramu; akapiga kambi mbele ya huo mji. Akainunua sehemu ya nchi, alipopiga hema yake, kwa mkono wa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa vipande mia vya fedha. Akajenga huko madhabahu, akaiita, El-elohe-Israeli.