Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Eze 43:13-27

Eze 43:13-27 SUV

Na vipimo vya madhabahu kwa dhiraa ni hivi; (dhiraa ni dhiraa na shubiri); tako lake ni dhiraa moja, na upana wake dhiraa moja; na pambizo yake karibu na ncha yake pande zote, shubiri moja; na hili litakuwa tako la madhabahu. Tena toka chini, juu ya nchi, hata daraja ya chini, dhiraa mbili, na upana wake dhiraa moja; tena toka daraja ndogo hata daraja kubwa, dhiraa nne, na upana wake dhiraa moja. Na madhabahu ya juu itakuwa dhiraa nne; na toka madhabahu pawashwapo moto na kwenda juu zitakuwa pembe nne. Na pale pawashwapo moto, urefu wake dhiraa kumi na mbili, na upana wake kumi na mbili, mraba pande zake nne. Na daraja, urefu wake dhiraa kumi na nne, na upana wake dhiraa kumi na nne, pande zake nne; na pambizo yake nusu dhiraa; na tako lake dhiraa moja, kote kote, na madaraja yake yataelekea upande wa mashariki. Kisha akaniambia, Mwanadamu, Bwana MUNGU asema hivi; Hizi ndizo sheria za madhabahu katika siku ile watakapoifanya, ili watoe sadaka za kuteketezwa juu yake, na kunyunyiza damu juu yake. Utawapa makuhani Walawi, walio wa uzao wa Sadoki, walio karibu nami, ili kunihudumu, asema Bwana MUNGU, ng’ombe mume mchanga awe sadaka ya dhambi. Nawe utatwaa baadhi ya damu yake, na kuitia juu ya pembe zake nne, na juu ya ncha nne za daraja, na juu ya pambizo yake pande zote; ndivyo utakavyoitakasa, na kuifanyia upatanisho. Tena utamtwaa ng’ombe wa sadaka ya dhambi, naye utamteketeza mahali palipoamriwa pa nyumba ile, nje ya mahali patakatifu. Na siku ya pili utamtoa beberu mkamilifu awe sadaka ya dhambi; nao wataisafisha madhabahu, kama walivyoisafisha kwa ng’ombe huyo. Utakapokwisha kuitakasa, utatoa ng’ombe mume mchanga mkamilifu, na kondoo mume wa kundini mkamilifu. Nawe utawaleta karibu mbele za BWANA, na makuhani watamwaga chumvi juu yao, nao watawatoa wawe sadaka za kuteketezwa kwa BWANA. Kwa muda wa siku saba utaweka tayari mbuzi kila siku awe sadaka ya dhambi; pia wataweka tayari ng’ombe mume mchanga, na kondoo mume wa kundini, wakamilifu. Kwa muda wa siku saba wataifanyia madhabahu upatanisho, na kuitakasa; ndivyo watakavyoiweka wakfu. Nao watakapozitimiza siku hizo, itakuwa, siku ya nane na baadaye, makuhani watatoa sadaka zenu za kuteketezwa juu ya madhabahu, na sadaka zenu za amani nami nitawakubali ninyi, asema Bwana MUNGU.