Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Dan 2:31-49

Dan 2:31-49 SUV

Wewe, Ee Mfalme, uliona, na tazama, sanamu kubwa sana. Sanamu hii, iliyokuwa kubwa sana, na mwangaza wake mwingi sana, ilisimama mbele yako; na umbo lake lilikuwa lenye kutisha. Na sanamu hii kichwa chake kilikuwa ni cha dhahabu safi; kifua chake na mikono yake ni ya fedha; tumbo lake na viuno vyake ni vya shaba; miguu yake ni ya chuma; na nyayo za miguu yake nusu ya chuma na nusu ya udongo. Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande. Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote. Hii ndiyo ile ndoto, nasi tutaihubiri tafsiri yake mbele ya mfalme. Wewe, Ee mfalme, u mfalme wa wafalme, na Mungu wa mbinguni amekupa ufalme, na uwezo, na nguvu, na utukufu; na kila mahali wakaapo wanadamu, wanyama wa kondeni na ndege wa angani amewatia mkononi mwako, naye amekumilikisha juu ya hao wote; wewe u kichwa kile cha dhahabu. Na baada ya zamani zako utainuka ufalme mwingine mdogo kuliko wewe; na ufalme mwingine wa tatu wa shaba, utakaoitawala dunia yote. Na ufalme wa nne utakuwa na nguvu mfano wa chuma; kwa maana chuma huvunja vitu vyote na kuvishinda; na kama chuma kisetavyo vitu hivi vyote, ndivyo utakavyovunja-vunja na kuseta. Na kama vile ulivyoziona hizo nyayo za miguu na vidole vyake, kuwa nusu udongo wa mfinyanzi, na nusu chuma, ufalme ule utakuwa ufalme uliogawanyika; lakini ndani yake zitakuwako nguvu za chuma, kama vile ulivyoona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope. Na kama vidole vya zile nyayo vilikuwa nusu chuma na nusu udongo, kadhalika ufalme ule utakuwa nusu yake una nguvu, na nusu yake umevunjika. Na kama vile ulivyokiona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope, watajichanganya nafsi zao kwa mbegu za wanadamu; lakini hawatashikamana, kama vile chuma kisivyoshikamana na udongo. Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele. Na kama vile ulivyoona ya kuwa jiwe lilichongwa mlimani bila kazi ya mikono, na ya kuwa lilivunja-vunja kile chuma, na ile shaba na ule udongo, na ile fedha, na ile dhahabu; basi Mungu aliye mkuu amemjulisha mfalme mambo yatakayokuwa baadaye; na ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti. Ndipo Nebukadreza, mfalme, akaanguka kifudifudi, akamsujudia Danieli, akatoa amri wamtolee Danieli sadaka na uvumba. Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, Hakika Mungu wenu ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme, awezaye kufumbua siri, kwa kuwa wewe uliweza kuifumbua siri hii. Basi mfalme akamtukuza Danieli, akampa zawadi kubwa nyingi sana, akamfanya kuwa mkubwa juu ya uliwali wote wa Babeli, na kuwa liwali mkuu juu ya wote wenye hekima wa Babeli. Tena, Danieli akamwomba mfalme, naye akawaweka Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wawe juu ya mambo yote ya uliwali wa Babeli; lakini huyo Danieli alikuwa akiketi katika lango la mfalme.