2 Sam 20:13-26
2 Sam 20:13-26 SUV
Na alipoondolewa katika njia kuu, watu wote wakapita, wakamwandama Yoabu ili kumfuatia Sheba, mwana wa Bikri. Naye akapita kati ya kabila zote za Israeli mpaka Abeli, na kwa Bethmaaka na Wabikri wote; nao wakakusanyika, wakaenda pia kumwandama. Na hao wakaja wakamhusuru katika Abeli wa Bethmaaka, wakafanya chuguu mbele ya mji, nayo ikasimama kuielekea ngome; na watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakavunja-vunja ukuta, wapate kuubomoa. Ndipo akalia mwanamke mmoja mwenye akili toka mjini, Sikieni, sikieni; mwambieni na Yoabu, aje hapa karibu, niseme naye. Basi akamkaribia; na yule mwanamke akasema, Ndiwe Yoabu? Akajibu, Ndimi. Ndipo akamwambia Sikia maneno ya mjakazi wako. Akajibu, Mimi nasikia. Kisha akanena, akisema, Watu hunena zamani za kale, wakisema, Wasikose kuuliza huko Abeli; ndivyo walivyomaliza shauri. Mimi ni wa hao wenye amani, walio waaminifu katika Israeli; wewe unatafuta kuuharibu mji, na mama wa Israeli; mbona wataka kuumeza urithi wa BWANA? Yoabu akajibu, akasema, Isiwe, isiwe kwangu, niumeze wala kuuharibu. Neno hili silo hivyo; lakini mtu mmoja wa milima ya Efraimu, Sheba, mwana wa Bikri, jina lake, ameinua mkono wake juu ya mfalme, naam, Daudi, basi mtoeni yeye tu, nami nitaondoka katika mji huu. Basi yule mwanamke akamwambia Yoabu, Tazama, kichwa chake utatupiwa juu ya ukuta. Ndipo yule mwanamke akawaendea watu wote katika akili zake. Nao wakamkata kichwa Sheba, mwana wa Bikri, wakamtupia Yoabu huko nje. Ndipo akapiga tarumbeta, nao wakatawanyika kutoka mjini kila mtu hemani kwake. Naye Yoabu akarudi mpaka Yerusalemu kwa mfalme. Basi Yoabu alikuwa juu ya jeshi lote la Israeli; na Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa juu ya Wakerethi, na juu ya Wapelethi; na Adoramu alikuwa juu ya shokoa; na Yehoshafati, mwana wa Ahiludi, alikuwa mkumbushi; na Shausha mwandishi; na Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani. Tena na Ira, Myairi, alikuwa kuhani kwa Daudi.