2 Fal 19:14-24
2 Fal 19:14-24 SUV
Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya BWANA, akaukunjua mbele za BWANA. Naye Hezekia akaomba mbele za BWANA, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, Ee BWANA, usikie; fumbua macho yako, Ee BWANA, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, BWANA, wafalme wa Ashuru wamewaharibu mataifa na nchi zao, na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu, ndiyo sababu wakaiharibu. Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA Mungu, wewe peke yako. Ndipo Isaya, mwana wa Amozi, akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akisema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa umeniomba juu ya Senakeribu, mfalme wa Ashuru, mimi nimekusikia. Tamko alilolitamka BWANA katika habari zake ndilo hili, Bikira, binti Sayuni, amekudharau, na kukudhihaki sana; binti Yerusalemu ametikisa kichwa chake juu yako. Ni nani uliyemshutumu na kumtukana? Umeinua sauti yako juu ya nani, na kuinua macho yako juu? Juu ya Mtakatifu wa Israeli. Kwa vinywa vya wajumbe wako umemshutumu Bwana, ukasema, Kwa wingi wa magari yangu nimepanda juu ya vilele vya milima, mpaka mahali pa ndani pa Lebanoni. Nami nitaikata mierezi yake mirefu, na misunobari yake mizuri; nami nitaingia ndani ya makazi yake yaliyo mbali sana, na msitu wa shamba lake lizaalo sana. Nimechimba na kunywa maji mageni, na kwa nyayo za miguu yangu nitaikausha mito yote ya Misri.