Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nya 34:1-18

2 Nya 34:1-18 SUV

Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, akaziendea njia za Daudi babaye, asigeuke kwa kuume wala kwa kushoto. Kwa kuwa katika mwaka wa nane wa kutawala kwake, naye akali mchanga, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi babaye; hata katika mwaka wa kumi na mbili akaanza kusafisha Yuda na Yerusalemu kwa kuondoa mahali pa juu, na kwa kuondoa maashera, na sanamu za kuchora, nazo za kusubu. Wakazibomoa madhabahu za mabaali machoni pake; na sanamu za jua, zilizoinuliwa juu yake, akazikata-kata; na maashera, na sanamu za kuchonga, nazo za kusubu, akazivunja-vunja, akaziponda kuwa mavumbi, akayamimina juu ya makaburi ya hao waliozichinjia dhabihu. Akaiteketeza mifupa ya makuhani madhabahuni mwao, akasafisha Yuda na Yerusalemu. Na katika miji ya Manase, na Efraimu, na Simeoni, mpaka Naftali, akafanya vile vile; na katika maganjo yake pande zote. Akazibomoa madhabahu, akaponda-ponda maashera na sanamu kuwa mavumbi, akazikata-kata sanamu zote za jua katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu. Hata katika mwaka wa kumi na nane wa kutawala kwake, alipokwisha kuisafisha nchi, na nyumba, akamtuma Shafani, mwana wa Azalia, na Maaseya, akida wa mji, na Yoa, mwana wa Yoahazi, mwandishi wa tarehe, waitengeneze nyumba ya BWANA, Mungu wake. Wakamjia Hilkia kuhani mkuu, wakampa fedha, iliyoletwa nyumbani mwa Mungu, waliyoikusanya Walawi, wangoje mlango, mikononi mwa Manase na Efraimu, na mabaki yote ya Israeli, na Yuda yote na Benyamini, na wenyeji wa Yerusalemu. Wakaitia mikononi mwa watenda kazi walioisimamia nyumba ya BWANA; na hao mafundi waliotenda kazi nyumbani mwa BWANA wakaitoa kwa kuitengeneza na kuifanya upya nyumba; wakawapa maseremala na waashi, ili wanunue mawe ya kuchonga, na miti ya kuungia, na kuifanyiza boriti kwa nyumba zile walizoziharibu wafalme wa Yuda. Nao watu wakatenda kazi kwa uaminifu; na wasimamizi wao walikuwa Yahathi na Obadia, Walawi, wa wana wa Merari; na Zekaria na Meshulamu, wa wana wa Wakohathi, ili kuihimiza kazi; na wengine katika Walawi, wote waliokuwa wastadi wa kupiga vinanda. Tena walikuwa juu ya wachukuzi wa mizigo, wakawahimiza wote waliotenda kazi ya huduma yo yote; na miongoni mwa Walawi kulikuwa na waandishi, na wasimamizi, na mabawabu. Nao walipotoa ile fedha iliyoletwa nyumbani mwa BWANA, Hilkia kuhani akakiona kitabu cha torati ya BWANA iliyotolewa kwa mkono wa Musa. Akajibu Hilkia akamwambia Shafani mwandishi, Kitabu cha torati nimekiona nyumbani mwa BWANA. Hilkia akampa Shafani kile kitabu. Shafani akampelekea mfalme hicho kitabu, tena akampasha mfalme habari, akisema, Yote waliyokabidhiwa watumishi wako, wayafanya. Nao wameimimina fedha iliyoonekana nyumbani mwa BWANA, nayo wameitia mikononi mwa wasimamizi, na mikononi mwa watenda kazi. Shafani mwandishi akamweleza mfalme, akisema, Hilkia kuhani amenipa kitabu. Shafani akasoma ndani yake mbele ya mfalme.