Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Sam 20:24-42

1 Sam 20:24-42 SUV

Basi Daudi akajificha shambani; na mwezi ulipoandama, mfalme aliketi kula chakula. Mfalme aliketi kitini mwake kama sikuzote, katika kiti kilichokuwa karibu na ukuta; Yonathani alikuwa mbele yake; Abneri naye akaketi karibu na Sauli; lakini mahali pake Daudi palikuwa hapana mtu. Lakini Sauli hakusema neno siku ile; maana alidhani ya kuwa, Amepatikana na neno, hakutakata; hakosi yeye hakutakata. Hata siku ya pili baada ya mwandamo wa mwezi, mahali pake palikuwa hapana mtu; basi Sauli akamwambia Yonathani mwanawe, Mbona mwana wa Yese haji kula chakula, jana wala leo? Naye Yonathani akamjibu Sauli, Daudi alitaka sana nimpe ruhusa aende Bethlehemu; akasema, Tafadhali nipe ruhusa niende; kwa maana jamaa yetu wana dhabihu mjini mwetu; na ndugu yangu ameniamuru niende; basi sasa, kama nimeona kibali machoni pako, nakuomba, niondoke; nikawatazame ndugu zangu. Ndiyo sababu hakuja mezani pa mfalme. Basi hasira yake Sauli ikawaka juu ya Yonathani, akamwambia, Wewe, mwana wa mke mkaidi, asi, je! Mimi sijui ya kuwa umemchagua huyo mwana wa Yese, kwa aibu yako mwenyewe, na kwa aibu ya uchi wa mama yako. Maana wakati mwana wa Yese akiwa hai juu ya nchi, wewe hutafanikiwa, wala ufalme wako. Basi, sasa peleka, ukamlete kwangu, maana hakika yake atakufa huyu. Yonathani akamjibu Sauli, baba yake, akamwambia, Auawe kwa sababu gani? Amefanya nini? Sauli akamtupia mkuki wake ili kumpiga; basi Yonathani akajua ya kuwa baba yake ameazimu kumwua Daudi. Basi Yonathani akaondoka pale mezani, mwenye hasira kali, wala hakula chakula siku ya pili ya mwezi, kwa sababu alimhuzunikia Daudi sana, na kwa sababu baba yake amemwaibisha. Hata asubuhi Yonathani akatoka kwenda shambani wakati ule alioagana na Daudi, na mtoto mdogo alikuwa pamoja naye. Akamwambia mtoto wake, Piga mbio, ukaitafute mishale niipigayo. Na yule mtoto alipokuwa akipiga mbio, akapiga mshale, ukapita juu yake. Na mtoto alipofika penye ule mshale alioupiga Yonathani, Yonathani akampigia mtoto kelele, akasema, Je! Mshale si huko mbele yako? Yonathani akampigia mtoto kelele, Haya! Hima! Usikawie. Mtoto wa Yonathani akaikusanya mishale, akaenda kwa bwana wake. Lakini yule mtoto hakujua lo lote. Yonathani na Daudi ndio walioijua habari yenyewe. Naye Yonathani akampa mtoto silaha zake, akamwambia, Nenda, ukazichukue mjini. Basi mara alipokuwa amekwisha ondoka yule mtoto, mara Daudi akatoka mahali pale karibu na kile kichuguu, akaanguka kifudifudi, akajiinama mara tatu; nao wakabusiana, wakaliliana, hata Daudi akazidi. Naye Yonathani akamwambia Daudi, Enenda kwa amani; kwa maana sisi sote wawili tumeapiana kwa jina la BWANA ya kwamba, BWANA atakuwa kati ya mimi na wewe, na kati ya uzao wangu na uzao wako milele. Daudi akaondoka, akaenda zake; Yonathani naye akaenda zake mjini.