Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Sefania 3

3
Maisha ya baadaye ya Yerusalemu
Hatima ya Yerusalemu
1Ole mji wa wadhalimu,
waasi na waliotiwa unajisi!
2Hautii mtu yeyote,
haukubali maonyo.
Haumtumaini Mwenyezi Mungu,
haukaribii karibu na Mungu wake.
3Maafisa wake ni simba wanaonguruma,
watawala wake ni mbwa-mwitu wa jioni,
ambao hawabakizi chochote
kwa ajili ya asubuhi.
4Manabii wake ni wenye kiburi,
ni wadanganyifu.
Makuhani wake hunajisi patakatifu
na kuihalifu sheria.
5Mwenyezi Mungu aliye ndani yake ni mwenye haki,
hafanyi kosa.
Asubuhi kwa asubuhi hutoa haki yake,
kila kukipambazuka huitimiza,
bali mtu dhalimu hana aibu.
Yerusalemu yakataa kutubu
6“Nimeyaangamiza mataifa,
ngome zao zimebomolewa.
Nimeziacha barabara ukiwa,
hakuna anayepita humo.
Miji yao imeharibiwa;
hakuna mmoja atakayeachwa:
hakuna hata mmoja.
7Niliuambia huo mji,
‘Hakika utaniogopa na kukubali maonyo!’
Ndipo makao yake hayatafutiliwa mbali,
wala adhabu zangu zote hazitakuja juu yake.
Lakini walikuwa bado na shauku
kutenda kwa upotovu katika yote waliyofanya.”
8Mwenyezi Mungu anasema,
“Kwa hiyo ningojee mimi,
siku nitakayosimama kuteka nyara.
Nimeamua kukusanya mataifa,
kukusanya falme
na kumimina ghadhabu yangu juu yao,
hasira yangu kali yote.
Dunia yote itateketezwa
kwa moto wa hasira yangu yenye wivu.
Mabaki ya Israeli kurejeshwa
9“Ndipo nitatakasa midomo ya mataifa,
kwamba wote waweze kuliitia jina la Mwenyezi Mungu
na kumtumikia kwa pamoja.
10Kutoka ng’ambo ya mito ya Kushi
watu wangu wanaoniabudu,
watu wangu waliotawanyika,
wataniletea sadaka.
11Siku hiyo hutaaibishwa
kwa ajili ya makosa yote uliyonitendea,
kwa sababu nitawaondoa kutoka mji huu
wale wote wanaoshangilia
katika kiburi chao.
Kamwe hutajivuna tena
katika kilima changu kitakatifu.
12Lakini nitakuachia ndani yako
wapole na wanyenyekevu,
ambao wanatumaini jina la Mwenyezi Mungu.
13Mabaki ya Israeli hayatafanya kosa;
hawatasema uongo,
wala udanganyifu hautakuwa
katika vinywa vyao.
Watakula na kulala
wala hakuna yeyote
atakayewaogopesha.”
14Imba, ee Binti Sayuni;
paza sauti, ee Israeli!
Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote,
ee Binti Yerusalemu!
15Mwenyezi Mungu amekuondolea adhabu yako,
amewarudisha nyuma adui zako.
Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Israeli, yu pamoja nawe;
kamwe hutaogopa tena madhara yoyote.
16Katika siku hiyo watauambia Yerusalemu,
“Usiogope, ee Sayuni;
usiiache mikono yako ilegee.
17Mwenyezi Mungu, Mungu wako, yu pamoja nawe,
yeye ni Shujaa mwenye nguvu anayeokoa.
Atakufurahia kwa furaha kubwa,
atakutuliza kwa pendo lake,
atakufurahia kwa kuimba.”
18“Huzuni katika sikukuu zilizoamriwa
nitaziondoa kwenu;
hizo ni mzigo na fedheha kwenu.
19Wakati huo nitawaadhibu
wote waliokudhulumu;
nitaokoa vilema na kukusanya
wale waliotawanywa.
Nitawapa sifa na heshima
katika kila nchi ambayo waliaibishwa.
20Wakati huo nitawakusanya;
wakati huo nitawaleta nyumbani.
Nitawapa sifa na heshima
miongoni mwa mataifa yote ya dunia
wakati nitakapowarudishia mateka yenu
mbele ya macho yenu hasa,”
asema Mwenyezi Mungu.

Iliyochaguliwa sasa

Sefania 3: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia