Ufunuo 9:1-12
Ufunuo 9:1-12 NEN
Malaika wa tano akaipiga tarumbeta yake, nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka toka angani hadi ardhini. Nyota hiyo ilipewa ufunguo wa lile Shimo. Alipolifungua hilo Shimo, moshi ukapanda kutoka humo kama moshi wa tanuru kubwa sana. Jua na anga vikatiwa giza na ule moshi uliotoka katika hilo Shimo. Ndipo katika ule moshi wakatoka nzige wakaenda juu ya nchi, nao wakapewa nguvu kama zile za nge wa duniani. Wakaambiwa wasidhuru nyasi ya nchi, wala mmea wala mti wowote, bali wawadhuru tu wale watu ambao hawana muhuri wa Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao. Wakaruhusiwa kuwatesa kwa muda wa miezi mitano, lakini wasiwaue. Uchungu wa kuuma kwao ulikuwa kama ule wa mtu aumwapo na nge. Katika siku hizo watu watatafuta kifo lakini hawatakiona, watatamani kufa, lakini kifo kitawakimbia. Wale nzige walikuwa na umbo kama la farasi waliotayarishwa kwa ajili ya vita. Kwenye vichwa vyao kulikuwa na kitu kama taji za dhahabu na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu. Walikuwa na nywele kama za wanawake, na meno yao yalikuwa kama ya simba. Walikuwa na dirii kama za chuma, na sauti za mabawa yao zilikuwa kama ngurumo za farasi wengi na magari mengi yakikimbilia vitani. Walikuwa na mikia yenye miiba ya kuumia kama nge. Nguvu yao ya kutesa watu kwa huo muda wa miezi mitano ilikuwa katika hiyo mikia yao. Walikuwa na mfalme wao, ambaye ni malaika wa lile Shimo, ambaye jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani ni Apolioni. Ole ya kwanza imepita, bado nyingine mbili zinakuja.