Ufunuo 17:7-11
Ufunuo 17:7-11 NENO
Ndipo yule malaika akaniambia, “Kwa nini unastaajabu? Nitakufafanulia siri ya huyo mwanamke na huyo mnyama aliyempanda, mwenye vichwa saba na pembe kumi. Huyo mnyama ambaye ulimwona awali alikuwako, lakini sasa hayuko, naye atapanda kutoka lile Shimo na kwenda kwenye maangamizi yake. Watu wanaoishi duniani ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima tangu kuumbwa kwa ulimwengu watastaajabu kumwona huyo mnyama, kwa maana alikuwako hapo awali, na sasa hayuko, lakini atakuwako baadaye. “Hapa ndipo penye wito wa akili pamoja na hekima. Vile vichwa saba ni vilima saba ambavyo huyo mwanamke amevikalia. Pia hivyo vichwa saba ni wafalme saba. Watano wamekwisha kuanguka, mmoja yupo, mwingine hajaja bado, lakini atakapokuja atalazimika kukaa kwa muda mfupi. Yule mnyama aliyekuwako hapo awali na sasa hayuko, yeye ni mfalme wa nane. Ni miongoni mwa wale saba, naye anaenda kwenye maangamizi yake.