Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 42

42
Kitabu cha Pili
(Zaburi 42–72)
Zaburi 42
Maombi ya mtu aliye uhamishoni
Kwa mwimbishaji. Utenzi wa wana wa Kora.
1Kama ayala anavyoonea shauku vijito vya maji,
ndivyo nafsi yangu inavyokuonea shauku, Ee Mungu.
2Nafsi yangu inamwonea Mungu kiu, Mungu aliye hai.
Ni lini nitaweza kwenda kukutana na Mungu?
3Machozi yangu yamekuwa chakula changu
usiku na mchana,
huku watu wakiniambia mchana kutwa,
“Yuko wapi Mungu wako?”
4Mambo haya nayakumbuka
ninapoimimina nafsi yangu:
Jinsi nilivyokuwa nikienda na umati wa watu,
nikiongoza maandamano kuelekea kwenye nyumba ya Mungu,
kwa kelele za shangwe na za shukrani
katikati ya umati wa watu waliosherehekea.
5Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka?
Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?
Weka tumaini lako kwa Mungu,
kwa kuwa bado nitamsifu,
Mwokozi wangu na Mungu wangu.
6Nafsi yangu inasononeka ndani yangu;
kwa hiyo nitakukumbuka
kutoka nchi ya Yordani,
katika vilele vya Hermoni,
kutoka Mlima Mizari.
7Kilindi huita kilindi,
katika ngurumo za maporomoko ya maji yako;
mawimbi yako yote pamoja na viwimbi
vimepita juu yangu.
8Mwenyezi Mungu huelekeza upendo wake mchana,
wimbo wake uko nami usiku:
maombi kwa Mungu wa uzima wangu.
9Ninamwambia Mungu Mwamba wangu,
“Kwa nini umenisahau?
Kwa nini niendelee kuomboleza,
nikiteswa na adui?”
10Mifupa yangu inateseka kwa maumivu makali
adui zangu wanaponidhihaki,
wakiniambia mchana kutwa,
“Yuko wapi Mungu wako?”
11Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka?
Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?
Weka tumaini lako kwa Mungu,
kwa kuwa bado nitamsifu,
Mwokozi wangu na Mungu wangu.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 42: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia