Zaburi 29:1-11
Zaburi 29:1-11 NEN
Mpeni BWANA, enyi mashujaa, mpeni BWANA utukufu na nguvu. Mpeni BWANA utukufu unaostahili jina lake; mwabuduni BWANA katika uzuri wa utakatifu wake. Sauti ya BWANA iko juu ya maji; Mungu wa utukufu hupiga radi, BWANA hupiga radi juu ya maji makuu. Sauti ya BWANA ina nguvu; sauti ya BWANA ni tukufu. Sauti ya BWANA huvunja mierezi; BWANA huvunja vipande vipande mierezi ya Lebanoni. Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama, Sirioni urukaruke kama mwana nyati. Sauti ya BWANA hupiga kwa miali ya umeme wa radi. Sauti ya BWANA hutikisa jangwa; BWANA hutikisa Jangwa la Kadeshi. Sauti ya BWANA huzalisha ayala, na huuacha msitu wazi. Hekaluni mwake wote wasema, “Utukufu!” BWANA huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika; BWANA ametawazwa kuwa Mfalme milele. BWANA huwapa watu wake nguvu; BWANA huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.