Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 119:1-96

Zaburi 119:1-96 NEN

Heri wale walio waadilifu katika njia zao, wanaoenenda katika sheria ya BWANA. Heri wale wanaozishika shuhuda zake, wamtafutao kwa moyo wao wote. Wasiofanya lolote lililo baya, wanaoenenda katika njia zake. Umetoa maagizo yako ili tuyatii kwa ukamilifu. Laiti mwenendo wangu ungekuwa imara katika kuyatii maagizo yako! Hivyo mimi sitaaibishwa ninapozingatia amri zako zote. Nitakusifu kwa moyo mnyofu ninapojifunza sheria zako za haki. Nitayatii maagizo yako; usiniache kabisa. BWANA Kijana aifanye njia yake kuwa safi jinsi gani? Ni kwa kutii, akilifuata neno lako. Ninakutafuta kwa moyo wangu wote, usiniache niende mbali na amri zako. Nimelificha neno lako moyoni mwangu ili nisikutende dhambi. Sifa ni zako, Ee BWANA, nifundishe maagizo yako. Kwa midomo yangu nitasimulia sheria zote zinazotoka katika kinywa chako. Ninafurahia kufuata sheria zako kama mtu afurahiaye mali nyingi. Ninatafakari maagizo yako na kuziangalia njia zako. Ninafurahia maagizo yako, wala sitalipuuza neno lako. BWANA Mtendee mema mtumishi wako, nami nitaishi; nitalitii neno lako. Yafungue macho yangu nipate kuona mambo ya ajabu katika sheria yako. Mimi ni mgeni duniani, usinifiche amri zako. Nafsi yangu inataabika kwa shauku kubwa juu ya sheria zako wakati wote. Unawakemea wenye majivuno, waliolaaniwa waendao mbali na amri zako. Niondolee dharau na dhihaka, kwa kuwa ninazishika sheria zako. Ingawa watawala huketi pamoja na kunisingizia, mtumishi wako atatafakari juu ya maagizo yako. Sheria zako ni furaha yangu, nazo ni washauri wangu. BWANA Nimelazwa chini mavumbini, yahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako. Nilikueleza njia zangu ukanijibu, nifundishe sheria zako. Nijulishe mafundisho ya mausia yako, nami nitatafakari maajabu yako. Nafsi yangu imechakazwa kwa huzuni, uniimarishe sawasawa na neno lako. Niepushe na njia za udanganyifu, kwa neema unifundishe sheria zako. Nimechagua njia ya kweli, nimekaza moyo wangu katika sheria zako. Nimengʼangʼania sheria zako, Ee BWANA, usiniache niaibishwe. Nakimbilia katika njia ya maagizo yako, kwa kuwa umeuweka moyo wangu huru. Ee BWANA, nifundishe kuyafuata maagizo yako, nami nitayashika mpaka mwisho. Nipe ufahamu, nami nitaishika sheria yako na kuitii kwa moyo wangu wote. Niongoze kwenye njia ya amri zako, kwa kuwa huko napata furaha. Ugeuze moyo wangu kuelekea sheria zako, na siyo kwenye mambo ya ubinafsi. Geuza macho yangu kutoka kwenye mambo yasiyofaa, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako. Mtimizie mtumishi wako ahadi yako, ili upate kuogopwa. Niondolee aibu ninayoiogopa, kwa kuwa sheria zako ni njema. Tazama jinsi ninavyoonea shauku mausia yako! Hifadhi maisha yangu katika haki yako. BWANA Ee BWANA, upendo wako usiokoma unijie, wokovu wako sawasawa na ahadi yako, ndipo nitakapomjibu anayenidhihaki, kwa kuwa ninalitumainia neno lako. Usilinyakue neno la kweli kutoka kinywani mwangu, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika amri zako. Nitaitii amri yako daima, naam, milele na milele. Nitatembea nikiwa huru, kwa kuwa nimejifunza mausia yako. Nitasema sheria zako mbele za wafalme wala sitaaibishwa, kwa kuwa ninazifurahia amri zako kwa sababu ninazipenda. Ninaziinulia amri zako ambazo ninazipenda mikono yangu, nami ninatafakari juu ya maagizo yako. BWANA Kumbuka neno lako kwa mtumishi wako, kwa sababu umenipa tumaini. Faraja yangu katika mateso yangu ni hii: Ahadi yako inahifadhi maisha yangu. Wenye majivuno wamenisimanga bila kuchoka, hata hivyo sitaiacha sheria yako. Ee BWANA, ninazikumbuka sheria zako za zamani, nazo zinanifariji. Nimeshikwa sana na ghadhabu kwa ajili ya waovu, ambao wameacha sheria yako. Maagizo yako ni kiini cha nyimbo zangu popote ninapoishi. Ee BWANA, wakati wa usiku ninalikumbuka jina lako, nami nitatii sheria yako. Hili limekuwa zoezi langu: nami ninayatii mausia yako. BWANA Ee BWANA, wewe ni fungu langu, nimeahidi kuyatii maneno yako. Nimetafuta uso wako kwa moyo wangu wote, nihurumie sawasawa na ahadi yako. Nimezifikiri njia zangu na nimeelekeza hatua zangu katika mausia yako. Nitafanya haraka bila kuchelewa kuzitii amri zako. Hata waovu wanifunge kwa kamba, sitasahau sheria yako. Usiku wa manane ninaamka kukushukuru kwa sababu ya sheria zako za haki. Mimi ni rafiki kwa wale wote wakuchao, kwa wote wanaofuata mausia yako. Ee BWANA, dunia imejaa upendo wako, nifundishe maagizo yako. BWANA Mtendee wema mtumishi wako Ee BWANA, sawasawa na neno lako. Nifundishe maarifa na uamuzi mzuri, kwa kuwa ninaamini amri zako. Kabla sijapata shida nilipotea njia, lakini sasa ninalitii neno lako. Wewe ni mwema, unalotenda ni jema, nifundishe maagizo yako. Ingawa wenye majivuno wamenisingizia uongo, nitafuata mausia yako kwa moyo wangu wote. Mioyo yao ni katili na migumu, bali mimi napendezwa na sheria yako. Ilikuwa vyema mimi kupata shida ili nipate kujifunza maagizo yako. Sheria inayotoka kinywani mwako ina thamani kubwa kwangu kuliko maelfu ya vipande vya fedha na dhahabu. BWANA Mikono yako ilinifanya na kuniumba, nipe ufahamu niweze kujifunza amri zako. Wakuchao wafurahie wanaponiona, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika neno lako. Ee BWANA, ninajua kwamba sheria zako ni za haki, katika uaminifu wako umeniadhibu. Upendo wako usiokoma uwe faraja yangu, sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. Huruma yako na inijie ili nipate kuishi, kwa kuwa naifurahia sheria yako. Wenye majivuno na waaibishwe kwa kunikosea mimi bila sababu, lakini mimi nitatafakari juu ya mausia yako. Wale wakuchao na wanigeukie mimi, hao ambao wanazielewa sheria zako. Moyo wangu usiwe na lawama katika kutii maagizo yako, ili nisiaibishwe. Nafsi yangu inazimia kwa kutamani wokovu wako, lakini nimeweka tumaini langu katika neno lako. Macho yangu yamefifia, nikingoja ahadi yako; ninasema, “Utanifajiri lini?” Ingawa nimekuwa kama kiriba kwenye moshi, bado sijasahau maagizo yako. Mtumishi wako itampasa angoje mpaka lini? Ni lini utawaadhibu washtaki wangu? Wenye majivuno wananichimbia mashimo, kinyume na sheria yako. Amri zako zote ni za kuaminika; unisaidie, kwa sababu watu wananishtaki bila sababu. Walikaribia kabisa kunifuta kutoka uso wa dunia, lakini sijaacha mausia yako. Yahifadhi maisha yangu sawasawa na upendo wako, nami nitatii sheria za kinywa chako. BWANA Ee BWANA, neno lako ni la milele, linasimama imara mbinguni. Uaminifu wako unaendelea kwa vizazi vyote, umeiumba dunia, nayo inadumu. Sheria zako zinadumu hadi leo, kwa kuwa vitu vyote vinakutumikia. Kama nisingefurahia sheria yako, ningeangamia katika taabu zangu. Sitasahau mausia yako kamwe, kwa maana kwayo umehifadhi maisha yangu. Uniokoe, kwa maana mimi ni wako, kwa kuwa nimetafuta mausia yako. Waovu wanangojea kuniangamiza, bali mimi ninatafakari sheria zako. Katika ukamilifu wote ninaona mna kikomo, lakini amri zako hazina mpaka.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zaburi 119:1-96