Wafilipi 4:14-23
Wafilipi 4:14-23 NEN
Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu. Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kanisa jingine lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi. Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja. Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu. Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi; nimetoshelezwa kabisa sasa, kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu. Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu. Mungu wetu aliye Baba yetu apewe utukufu milele na milele. Amen. Msalimuni kila mtakatifu katika Kristo Yesu. Ndugu walioko pamoja nami wanawasalimu. Watakatifu wote wanawasalimu, hasa wale watu wa nyumbani mwa Kaisari. Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.